SOMO: Maombi Yasiyojibiwa (Na Imani)
Fungu Elekezi: “Bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya”
Isa. 40:31a).
Kungojea …
Kusubiri si kitu cha kufurahisha. Nani anapenda kusubiri? Kusubiri katika ofisi ya daktari, kusubiri mstarini, kusubiri ndege iliyochelewa kwenye uwanja wa ndege, kusubiri mtu ambaye amechelewa kwenye mkutano.
Ibrahimu alilazimika kusubiri kwa miaka 25 ili kupata majibu ya ombi lake. Musa alingoja miaka 40 ili Mungu aingilie kati hatimaye. Yusufu alikuwa mtumwa kwa miaka kadhaa kisha akakaa gerezani miaka michache—si mahali pa kufurahisha pa kungojea kuingilia kati kwa Mungu! Kuna mifano mingi ya kusubiri msaada katika Biblia.
Japokuwa kungojea huleta changamoto kwenye subira yetu, Biblia inasema kwamba sifa moja ya watu wa Mungu ni subira. Vivyo hivyo katika maombi. Mara nyingi, tunalazimika kusubiria majibu.
“Kila ombi la dhati hupata majibu. Jibu linaweza lisije katika namna ambayo unaipenda, au kwa wakati ambao unalitegemea; lakini litakuja kwa njia na kwa wakati ambao litakidhi mahitaji yako. Maombi unayofanya peke yako, ukiwa umechoka, ukiwa majaribuni, Mungu anayajibu, siyo daima kulingana na matarajio yako, lakini daima kwa ajili ya maslahi yako” (Messages to Young People, uk. 250).
Tunapojinyenyekeza na kuwasilisha hitaji letu, kwa njia iliyo wazi, dhahiri, tukikiri utegemezi wetu kamili kwa Mungu, Yeye hujibu. Hata hivyo, mara nyingi tunapaswa kusubiri. Mara nyingi tunahitaji kutumia uwezo na chaguzi zetu zote kabla ya Mungu kuingilia kati, ili tuweze kujua kwa uhakika kwamba alikuwa ni Yeye.
Kama Yeye angelijibu mara moja, tungaliweza kuchukua sifa kwa ajili yetu wenyewe.
Tunapoona hakuna njia iwezekanayo ya kutatua mgogoro, Mungu husema neno, na jambo ambalo hatukuweza kuwaza linatokea. “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua” (Yer. 33:3).
Hata hivyo, ikiwa Mungu hatajibu kwa wakati huo na kwa njia tuombayo, tunaweza kufikiri kwamba hakujibu kabisa. Mungu hujibu maombi ya dhati, ya unyenyekevu na jibu Lake ndilo jibu bora zaidi.
Umeitwa ili kuujua upendo wa Mungu (Efe. 3:19). Hiyo ndiyo yote unayohitaji. Kadiri unavyomjua zaidi, ndivyo unavyomwamini zaidi, ndivyo unavyokuwa na amani zaidi na ndivyo unavyokuwa tayari kungoja uongozi Wake na kuingilia kati Kwake. Kaza macho yako Kwake, katika upendo Wake, ahadi Zake na kwa njia ambayo Ameongoza katika changamoto zilizopita.
“Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea” (Isa. 26:3).
Mungu anaujua wakati ujao. Anakujali, lakini pia anawajali wengine. Anaweza asijibu sasa kwa sababu Analo jibu bora zaidi au si wakati mzuri zaidi, au hauko tayari kwa mpango Wake. Anaweza kuwa na jibu tofauti ambalo linashughulikia mahitaji mengine, mambo ambayo huwezi kuyafikiria. Anaweza pia kuruhusu kitu fulani maishani mwako kama njia pekee ya kumfikia mtu ambaye vinginevyo hangefikiwa. Mambo mengi yanatokea ambayo tutayaelewa mbinguni tu.
Zingatia kwamba, Yesu hakuja na kufa ili kutupatia maisha ya starehe duniani. Kwa kweli, alisema kwamba katika ulimwengu huu tutapata majaribu (Yohana 16:33). Mara nyingi hutumia majaribu ili kutufundisha masomo muhimu kwa ajili ya ukuaji wa tabia na wokovu. “Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana” (2 Kor. 4:17).
Kwa hiyo badala ya kumwomba Mungu ili aondoe changamoto, mwombe Yeye ili akusaidie kukua na kujifunza kupitia hizo. Hitaji letu kuu zaidi si mahitaji tuyaombayo, japokuwa mara nyingi ni mahitaji halisi. Hitaji letu kuu ni kumjua Mungu wetu. Kadiri unavyomjua zaidi, ndivyo unavyomwamini zaidi na ndivyo unavyomruhusu zaidi kufanya kazi.
Mungu anakuita kuomba na kumtafuta Yeye, tafuta uwepo Wake, mpango Wake, uongozi Wake. Tafuta kumjua kabla ya kutafuta majibu na msaada, kisha telekeza juu Yake wasiwasi wako wote na umngoje Bwana.
Hebu na Tuombe Pamoja
Muda wa Maombi (Dakika 30–45)
Vikundi vyote vya maombi vina njia tofauti za kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja, kwa njia yoyote ambayo Roho Mtakatifu anaongoza. Tunahimiza maombi mafupi ya wazi (sentensi 1-3). Hii inaruhusu watu wengi zaidi kuomba mara nyingi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuomba kupitia Maandiko kulingana na mada. Unaweza kuomba kupitia vifungu vingine pia na kujumuisha masomo mengine katika wakati wako wa maombi. Tazama Mwongozo wa Kiongozi na Maombi ya Maombi ya Kanisa Ulimwenguni kwa mawazo ya maombi.
Kuomba Sawasawa na Neno la Mungu—Isa. 40:31a “Bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya” “Wao Wamngojeao Bwana”
Baba, huwa hatupendi kungojea. Kungoja hutufanya tuwe na wasiwasi na woga, kwa hiyo kwa haraka tunasonga mbele na kutafuta suluhu zetu wenyewe. Utufundishe kutulia ndani yako kama vile mtoto apumzikavyo mikononi mwa baba yake. Tupe imani ya kujua kwamba unaishikilia kesho katika mikono Yako yenye nguvu. Tuweze kuishi kwa imani, si kwa kuona.
“Watapata Nguvu Mpya”
Bwana, wakati mwingine tunachoshwa na maisha katika ulimwengu huu usio na matumaini. Tumechoshwa na magonjwa, kutoelewana, umaskini, ukosefu wa haki, na upweke. Tafadhali inua macho yetu mbinguni na ufanye upya nguvu zetu. Tufundishe kukutegemea Wewe na kupata nguvu katika ahadi Zako zisizo na mwisho. Tunapokuwa dhaifu, tuunganishe na uwezo Wako.
Mapendekezo ya Maombi Zaidi
Shukrani na Sifa: Shukuruni kwa baraka mahususi na Msifuni Mungu kwa wema Wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na umshukuru Mungu kwa msamaha Wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya Eneo Mahalia: Ombea mahitaji ya sasa ya washiriki wa kanisa, familia na majirani.
Sikiliza na Uitike: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa na nyimbo.
Mapendekezo ya Nyimbo
- Furaha Gani (Vk. 251 & Vd. 43)
- Ni Salama Rohoni (Vk. 327 & Vd. 127)