Ufalme Wako Uje
Fungu Elekezi: “Ufalme wa Mungu umo ndani yenu” (Luka 17:21b).
Wokovu Umeingia
Katika Luka 19 anajitolea kuingia katika nyumba ya Zakayo. Kisha Yesu anasema, “Leo wokovu umefika nyumbani humu” (aya ya 9). Yesu anapoishi nyumbani mwako, mbingu yote iko hapo. Na kabla hujauingia ufalme wa Mungu, lazima ufalme wa Mungu uingie moyoni mwako. Katika Yohana 17 Yesu hakuomba kwamba wafuasi Wake waondolewe kimwili kutoka ulimwenguni bali kwamba wasiwe wa ulimwengu (Yohana 17:15, 16).
Lazima tuzoee kuishi hapa leo kama ambavyo tutaishi mbinguni. Ikiwa tunajikita kwa mambo ya ulimwengu, tutakuwa kama ulimwengu. “Hazina yako ilipo, ndipo na moyo wako utakapokuwapo” (Mt. 6:21). Lakini kama tukijikita kwa Mungu na kwenye ufalme Wake, ufalme Wake utakuwa ndani yetu na karibu nasi. “Nyuso za wanaume na wanawake wanaozungumza na Mungu, ambaye ulimwengu usioonekana ni halisi kwao, huonesha amani ya Mungu. Wanabeba pamoja nao angahewa la mbinguni kunjufu na la kupendeza” (Medical Ministry, uk. 252).
Kwenye safari moja ya kiuinjilisti nchini Kuba, watoto wengi pamoja na wazazi wao walikuja kusikiliza. Nilifahamu kutoka kwa mchungaji kwamba wageni hawa wote walikuja kwa sababu ya mwanamke mmoja. Nilimwuliza ni nini alichokisema ili kuwafanya waje. Akanijibu, “siyo kile nilichowaambia,” na kisha akatualika tumtembelee siku iliyofuata na kuangalia. Kwa hiyo tulienda.
Alikuwa na nyumba ndogo sana, kama kibanda cha kutunzia vifaa. Hakukuwa na samani ndani isipokuwa vitanda viwili vya dabodeka, meza
ndogo, viti viwili vidogo na jiko la kukambikia. Mapema mchana alitoka nje mbele ya nyumba yake. Na kisha wakaja—takribani watoto mia mbili! Aliwaketisha chini mavumbini na kumwonesha karatasi zilizosainiwa na wazazi wao. Kisha watoto walipanga msitari na akawagawia wali wote. Wakaketi chini na kula.
Walipokuwa wanakula, alitueleza kwamba jirani zake wengi hawakuwa na ajira, lakini alikuwa amebarikiwa kuwa nayo. Mshahara wake usingetosha kununua vyakula vya aina mbalimbali, bali aliweza kununua mchele. Na kisha akasema, “Tumeitwa kuwa kama Yesu, ili kuonesha jinsi ulivyo ufalme wa Mungu kwa hiyo watu wanauhitaji. Tunapaswa kutumia mbinu ya Yesu. Kuwalisha na kujenga urafiki. Ikiwa ninaishi kwa ajili yangu, ninakuwaje kama Yesu? Na ikiwa ninawapa tu watu mkate wa kimwili, unawezaje kuwasaidia? Kwa hiyo ninatumia ubwabwa ili kuwaonesha watoto upendo. Kisha ninawapa pia mkate wa kiroho. Lakini watoto mara nyingi huhamishwa mawazo yao. Ili kuhakikisha kwamba watoto wanasikiliza, lazima waende nyumbani na, kama uthibitisho kwamba walizingatia, wawaambie wazazi wao kisa na wimbo waliojifunza leo. Kwa njia hii ninawafikia pia wazazi wao. Sasa kwa sababu nimekuwa nikifanya hivi kwa muda, wote wananipenda, wananiamini na wako tayari kusikiliza.”
Punde tu watoto walipomaliza kula, alianza kuwafundisha kuhusu Yona na kisha aliwafundisha wimbo. Baada ya hapo, walimkumbatia na kumshukuru. Niliwasikia wakisema, “Tunakupenda mama!” Alikuwa na tabasamu kubwa usoni mwake. Akasema, “Siyo hivyo tu kwamba ninajaribu kuwaonesha ufalme wa Mungu, lakini pia wananibariki na kunijaza furaha pia. Furaha yangu kubwa ni kuwaona wakija kanisani na kuomba na kumjifunza Mungu. Lakini furaha yangu kuu zaidi itakuwa ni kuwaona mbinguni. Kwa hiyo ninataka wapate muonjo kidogo wa mbinguni sasa.”
Yesu anakuja hivi karibuni! Lakini kwa wewe kuwa tayari kuuingia ufalme Wake pale atakapokuja, lazima uwe na ufalme Wake ukiishi
Siku 10 za Maombi 65
ndani yako sasa. Lazima uombe kila siku, “Bwana, naomba uje na ufalme Wako ndani ya moyo wangu leo.” Mungu anakuita kuufanya ufalme Wake kuwa halisi leo. Kwa njia ya maombi, usomaji wa Neno la Mungu na huduma ya furaha, ishi hapa kama utakavyo kuishi mbinguni. Iruhusu mbingu ikae ndani yako. Kuwa mkono wa Mungu hapa, kama ambavyo watu wa Imani walikuwa mikono Yake hapo kale.
Mungu anataka kuhamishia ufalme Wake moyoni na nyumbani mwako leo na kila siku. Anakutaka uzoee kuishi katika uwepo Wake kama raia wa mbinguni. Kila siku ialike mbingu ndani ya moyo wako na kuruhusu upendo Wake umwagike kwa wengine kupitia matendo yako.
Hebu Tuombe Pamoja
Muda wa Maombi (Dakika 30–45)
Vikundi vyote vya maombi vina njia tofauti za kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja, kwa njia yo yote ambayo Roho Mtakatifu anaongoza. Tunahimiza maombi mafupi ya wazi (sentensi 1-3). Hii inaruhusu watu wengi zaidi kuomba mara nyingi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuomba kupitia Maandiko kulingana na mada. Unaweza kuomba kupitia vifungu vingine pia na kujumuisha masomo mengine katika wakati wako wa maombi. Tazama Mwongozo wa Kiongozi na Maombi ya Maombi ya Kanisa Ulimwenguni kwa mawazo ya maombi.
Kuomba Sawasawa na Neno la Mungu—Luka 17:21b
“Ufalme wa Mungu umo ndani yenu”
“Ufalme wa Mungu”
Bwana, tunajua ufalme Wako si juu ya mamlaka au nguvu za ulimwengu. Utupe hekima ya kuelewa na kuuishi ufalme wako mtulivu katika maisha yetu leo. Tukamilishe ili tutumike, ili tufariji, na kuwatia moyo watoto Wako wa duniani.
“Umo Ndani Yenu”
Baba Mungu, tunaomba utusaidie kuishi kama raia wa mbinguni kuanzia leo. Geuza macho yetu kutoka kwetu ili tuwaangalie wengine. Ni mtu gani karibu nasi anahitaji sikio la kumsikiliza hivi sasa? Nani anahitaji chakula cha ukarimu au nguo kwa ajili ya watoto wao? Nani anahitaji kusikia ushuhuda wetu kuhusu nguvu ya Yesu inayobadilisha? Zungumza na mioyo yetu na usimamishe ufalme Wako katika maisha yetu leo.
Mapendekezo ya Maombi Zaidi
Shukrani na Sifa: Shukuruni kwa baraka mahususi na Msifuni Mungu kwa wema Wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na umshukuru Mungu kwa msamaha Wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya Eneo Mahalia: Ombea mahitaji ya sasa ya washiriki wa kanisa, familia na majirani.
Sikiliza na Uitike: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa na nyimbo.
Mapendekezo ya Nyimbo
- Tawala ndani Yangu (Vk. 339 & Vd. 147)
- Yu Hai, Yu Hai (Vk. 93 & Vd. 167)
