Mapenzi Yako Yatimizwe Hapa Duniani Kama Huko Mbinguni
Fungu Elekezi: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho” (Yeremia 29:11).
Yeye ni Bwana
Wote tunayo mipango, ya muda mrefu na ya kila siku. Katika maombi yetu mara nyingi tunamwomba Mungu kusaidia na kubariki mipango yetu badala ya kutafuta mipango ya Mungu. Mungu anasema, “Nayajua mawazo ninayowawazia ninyi” (Yeremia 29:11). Ili kupata baraka na uwezo wa Mungu, lazima ufuate mpango Wake.
Katika maombi tunamwagiza Mungu kufanya kana kwamba sisi ni bwana na Yeye ni mtumwa. Kumbuka kuwa, Yeye ni Mungu, Yeye ni Bwana. Anapaswa kutuagiza nini cha kufanya. Kila siku jiweke wakfu kwa Mungu kwa ajili ya siku hiyo. Salimisha mipango yako yote Kwake, ili itimilizwe au ili itolewe kama ambavyo mapenzi Yake yataonesha. Ndivyo ambavyo siku kwa siku utakuwa ukiyatoa maisha yako kwenye mikono ya Mungu” (Steps to Christ, uk. 70).
Kumbuka usemi huu katika sala ya Bwana: “Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni.” Huko mbinguni malaika wanamtumikia Mungu. Anawapatia kazi ya kufanya, nao wanaifanya. Jibu lao ni hili, “Ndiyo, Bwana,” na kisha wanaenda kufanya. Hakuna hata mmoja wao anayemwambia Mungu nini cha kufanya; hakuna anayehoji au kusema, “nina kazi nyingi” au “nitaifanya baadaye.” Hakuna anayelalama kwa kusema, “Sina uwezo” au Ninalo wazo jema zaidi.” Anapomwambia malaika kufanya kitu, wanafanya, wakijua kwamba Yeye anatoa uweza wote muhimu wanaouhitaji.
Siku moja mimi na mke wangu tulikuwa na safari ya kuendesha kwa saa kumi na moja. Kama kawaida, tuliomba mpango wa Mungu kwa ajili ya siku hiyo na kumwomba Yeye atuoneshe fursa za kutumika. Takribani saa tano baadaye tukiwa safarini, mchungaji rafiki mwema alinipigia simu. “Niombee,” alisema. Ninapaswa kwenda Kuba kwa ajili ya uinjilisti, lakini gari langu limeharibika na basi halikuja.”
Nilijua kuwa alikuwa akiishi katika eneo tulikokuwa tunapita wakati huo, kwa hiyo nilisema, “kwani unaishi wapi katika eneo hili?” Alinielekeza pa kuingilia. Tulipokuwa bado tunaongea, nilifika mahali pa kuingilia. “Tumefika hapa!” Nilisema kwa mshangao. “Inawezekanaje?” aliuliza. “Unaishi umbali wa kuendesha gari kwa saa tano kutoka kwangu upande wa kaskazini!” Tulifuata njia ile, tukafika nyumbani kwake, tukamchukua na kumpeleka mpaka uwanja wa ndege. Akapanda ndege na kwenda zake Kuba!
Mara nyingi tumeendelea kujitahidi na kushindwa katika juhudi zetu kwa sababu tunatenda kwa mipango yetu wenyewe. Lakini, hatujui vizuri kila kitu. Hatujui yajayo. Mungu anajua na Anatupenda.
“Wengi sana, katika kupanga kwa ajili ya siku njema zijazo, hushindwa kabisa. Mruhusu Mungu akupangie…. Mungu kamwe hawaongozi watoto Wake kinyume na vile ambavyo wangechagua kuongozwa, kama wangeweza kuona mwisho tangu mwanzo na kutambua utukufu wa kusudi wanalolitimiza kama watendakazi pamoja na Yeye” (The Ministry of Healing, uk. 479).
Ili kuyafanya mapenzi ya Mungu ni lazima uyafahamu, kwa hiyo unapaswa pia kusikiliza uwapo katika maombi. Kile Mungu anachokuambia ni muhimu zaidi kuliko kile unachomweleza. Sisi “tunapaswa kuwa na uzoefu binafsi katika kupata kujua mapenzi ya Mungu. Tunalazimika kila mmoja kumsikia Yeye akizungumza moyoni. Wakati kila sauti imenyamazishwa na katika ukimya tunamngoja Yeye, ukimya wa roho unaifanya sauti ya Mungu kusikika vizuri” (The Ministry of Healing, uk. 58).
Kwa njia ya maombi tunazungumza na Mungu, na kwa njia ya Neno Mungu anasema nasi. Maombi na usomaji wa Neno daima huenda pamoja; kamwe havipaswi kutenganishwa. Biblia ni sauti ya Mungu akisema nasi, dhahiri tu kama vile ambavyo tungeisikiliza kwa masikio yetu” (Testimonies for the Church, vol. 6, uk. 393).
Kwa hakika tunaweza kumwambia Yeye mahitaji yetu. Tunaambiwa kuweka mahitaji yetu yote juu Yake (1 Petro 5:7). Hakuna kosa lolote katika kumwomba msaada. Hata hivyo, haumjulishi Mungu kuhusu jambo ambalo bado halijui; badala yake, unampatia Yeye ukubali wako ili akusaidie. Mungu alitupatia uhuru wa kuchagua na anaheshimu chaguzi zetu. Kamwe hataingilia kati kwa kulazimisha mapenzi Yake kwetu. Anatusubiria mpaka pale tunapoomba, tunapochagua msaada Wake na kisha huingilia kati.
Omba, soma Neno, litafakari Neno. Wasilisha mahitaji na mipango yako na uombe kwa ajili ya maelekezo na mwongozo. Ifanye mipango ya Mungu kuwa kipaumbele chako. Mtafute Mungu kwanza, kisha uamini kwamba atakupatia mahitaji yako yote kama alivyoahidi (Mt. 6:33). Kuwa tayari kumtumikia na kufuata mapenzi Yake. Sema, “Mimi hapa Bwana. Unitumie leo. Mapenzi Yako yatimizwe katika maisha yangu leo.”
Hebu Tuombe Pamoja
Muda wa Maombi (Dakika 30 – 45)
Vikundi vyote vya maombi vina njia tofauti za kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja, kwa njia yo yote ambayo Roho Mtakatifu anaongoza. Tunahimiza maombi mafupi ya wazi (sentensi 1-3). Hii inaruhusu watu wengi zaidi kuomba mara nyingi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuomba kupitia Maandiko kulingana na mada. Unaweza kuomba kupitia vifungu vingine pia na kujumuisha masomo mengine katika wakati wako wa maombi.
Tazama Mwongozo wa Kiongozi na Maombi ya Maombi ya Kanisa Ulimwenguni kwa mawazo ya maombi.
Kuomba Sawasawa na Neno la Mungu—Yeremia 29:11.
”Kwa kuwa Nayajua mawazo ninayowawazia ninyi…. Ya kuwapa tumaini siku zenu za Mwisho.”
“Maana Nayajua Mawazo Ninayowawazia Ninyi”
Bwana, tunajishughulisha sana na mawazo yetu wenyewe. Tunaomba Utusamehe kwa tamaa, uchoyo na ubinafsi. Badala yake, tuoneshe mipango Yako. Elekeza macho yetu kuona mahitaji yanayotuzunguka. Fanya mikono na miguu yetu iwe tayari kutumika.
“Mawazo ya Kuwapa Tumaini Siku za Mwisho”
Baba Mungu, mipango yetu ya kidunia itasambaratika na kubatilika, lakini mipango Yako inadumu hata umilele. Asante kwamba kushindwa kwetu siyo kwa kudumu. Tupe imani ya kuutazama ufalme Wako leo. Ishi maisha Yako ndani yetu.
Mapendekezo ya Maombi Zaidi
Shukrani na Sifa: Shukuruni kwa baraka mahususi na Msifuni Mungu kwa wema Wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na umshukuru Mungu kwa msamaha Wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya Eneo Mahalia: Ombea mahitaji ya sasa ya washiriki wa kanisa, familia na majirani.
Sikiliza na Uitike: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa na nyimbo.
Mapendekezo ya Nyimbo
- Yote Namtolea Yesu (Vk. 332 & Vd. 122)
- Twae Wangu Uzima (Vk. 163 & Vd. 146)
