Usitutie Majaribuni
Fungu Elekezi: “Maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu” (Yakobo 1:13).
Je! Mungu Anafanya Hivyo Kweli?
Mungu ni mtakatifu, Yeye ni upendo. Hamjaribu mtu awaye yote, tunajitia wenyewe majaribuni (Yakobo 1:14, 15). Kwa hiyo sasa, umewahi kujiuliza kwamba Yesu alimaanisha nini aliposema katika Sala ya Bwana, “Usitutie majaribuni”? Yesu hakuwa anamaanisha kwamba Mungu hutujaribu mpaka tutende dhambi na kwamba ni lazima tumwombe ili asitusukumie majaribuni.
Kwa hiyo, ina maana gani? Kama ilivyo katika lugha nyingi kama siyo zote, maneno yanaweza kuwa na maana zaidi ya moja katika Kiyunani. Kwa hiyo ni lazima uangalie kwenye lugha ya asili na muktadha wake. Neno la Kiyunani “ongoza (tia)” ni eisphero. Aya hii inaweza kutafsiriwa kama “usituruhusu kwenda, usitutelekeze hapo, usitupatie ruhusa ya kwenda.” Haimaanishi “kushawishi.”
Neno la Kiyunani kwa “majaribu” ni peirasmon. Linaweza kufasiriwa kama “jaribio, tahini, taabu,” n.k. Kwa hiyo aya “usitutie majaribuni” inaweza kumaanisha, “Tafadhali usinitelekeze kwa sababu peke yangu nitasererekeadhambini, aukubakikatikadhambiambakonilishasererekea” au “ikiwa unanitahini, usiniache peke yangu wala kuniruhusu kubakia humo kwa muda mrefu kwa maana naogopa kudumbukia dhambini.”
Wakati fulani Mungu anaruhusu au kukuweka katika mahali mahususi ili kukusaidia kuelewa moyo wako na hali yako ya kiroho, kufumbua macho yako kuona jinsi ulivyo na kile unachohitaji. Biblia inasema kwamba wewe “hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka,
na maskini, na kipofu, na uchi” (Ufu. 3:17). Unapojua kuwa wewe ni mgonjwa, unakwenda kwa dakitari, lakini unawezaje kushughulikia jambo ambalo hulifahamu?
Tunapoona vile tulivyo, tunagundua jinsi tulivyo wenye dhambi na kujua kuwa tunamhitaji Yesu. “Wanaoishi karibu kabisa na Yesu wanatambua kwa uwazi zaidi udhaifu na hali ya dhambi ya mwanadamu, na tumaini lao pekee linapatikana katika haki ya Mwokozi aliyesulubiwa na aliyefufuka” (Pambano Kuu, uk. 389, 390).
Mungu alimpa jaribio Mfalme Hezekia (2 Nyakati 32:31). Mithali 17:3 inasema kwamba, Mungu huijaribu mioyo. Daudi aliomba, “Ee Bwana, unijaribu na kunipima” (Zab. 26:2). Petro anasema kwamba majaribio makali wakati mwingine yanalenga kututahini (1 Petro 4:12).
“Kuziona dhambi zetu kunatusukuma Kwake Yeye anayeweza kusamehe; wakati nafsi, inapotambua unyonge wake, inapomwendea Yesu, atajidhihirisha katika uweza” (Steps to Christ, uk. 65).
Kwa hiyo, “Adui yetu mkuu anatafuta daima kuiweka nafsi inayotaabika mbali na Mungu” (Prayer, uk. 270). Anajua kwamba tukitengwa mbali na Mungu, tutasererekea dhambini.
Katika sehemu ya mwisho ya Sala ya Bwana, Yesu anajaribu kuwekea mkazo siri ya nguvu na ushindi. Anasema kwamba tumaini letu pekee linapaswa kuwapo daima ndani ya Yesu na kuwa na Yesu ndani yetu, kutotengana kamwe na kutoachana kamwe. “Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu” (Kol. 1:27).
Peke yetu hatuna uwezo wa kubadilisha na kukuza moyo mpya. Lakini ahadi iko wazi na thabiti: “mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya” (2 Kor. 5:17).
Kwa hivyo unajiangaliaje ili kuona mahali ulipo katika safari yako ya kiroho? Yesu anasema tunaweza kujua kwa matunda yetu (Mt. 7:16).
Unawezaje kuzaa matunda? Kwa kuwa umeunganishwa daima pamoja na Yesu (Yohana 15:1–5) na kujazwa na Roho Wake (Gal. 5:22, 23).
“Kuikiri dini kunawaweka watu katika kanisa, lakini tabia na mwenendo unaonesha kama wanao uhusiano wa kudumu na Kristo” (The Desire of Ages, uk. 676). Ili uendelee kubaki ndani Yake, hauhitaji kufahamu jinsi anavyotenda; unachohitaji ni kumwamini tu. Anawaokoa wale wote wanaomjia Yeye (Ebr. 7:25).
“Ulinzi pekee dhidi ya uovu ni uwepo wa Yesu moyoni” (The Desire of Ages, uk. 324).
Mungu anakuita ili kuomba bila kukoma, kudumu kuliitia Jina la Bwana, kutembea pamoja Naye na katika utambuzi wa uwepo Wake daima na utegemezi kamili juu Yake na kutotengwa mbali Naye kamwe. Hiyo ndiyo nguvu yako pekee. Na anaahidi kwamba mkimkaribia Mungu, “Naye atawakaribia ninyi” (Yakobo 4:8).
Hebu Tuombe Pamoja
Muda wa Maombi (Dakika 30–45)
Vikundi vyote vya maombi vina njia tofauti za kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja, kwa njia yo yote ambayo Roho Mtakatifu anaongoza. Tunahimiza maombi mafupi ya wazi (sentensi 1-3). Hii inaruhusu watu wengi zaidi kuomba mara nyingi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuomba kupitia Maandiko kulingana na mada. Unaweza kuomba kupitia aya nyingine pia na kujumuisha masomo mengine katika wakati wako wa maombi. Tazama Mwongozo wa Kiongozi na Maombi ya Maombi ya Kanisa Ulimwenguni kwa mawazo ya maombi.
Kuomba Sawasawa na Neno la Mungu—Yakobo 1:13.
“Maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.”
“Mungu Hawezi Kujaribiwa na Uovu”
Baba, tunakushukuru kwa kumtuma Yesu kuupinga na kuushinda uovu kwa niaba yetu. Kwako hakuna giza hata kidogo, ila wema na nuru. Tunajua kwamba tayari umeshaishinda dhambi na mauti na kwamba unatubadilisha ili tufanane na Wewe. Yafanye macho yetu kukitwa kwako!
“Wala Yeye Mwenyewe Hamjaribu Mtu”
Bwana, tafadhali usituruhusu tubaki katika majaribu ambayo yanaweza kututenga mbali nawe. Tufundishe kuzikimbia tamaa za ubinafsi zinazotushawishi na kuelekeza macho yetu kwenye tabia Yako isiyo na doa. Tuwezeshe kuchukia kile unachokichukia na kupenda kile unachokipenda.
Mapendekezo ya Maombi Zaidi
Shukrani na Sifa: Shukuruni kwa baraka mahususi na Msifuni Mungu kwa wema Wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na umshukuru Mungu kwa msamaha Wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya Eneo Mahalia: Ombea mahitaji ya sasa ya washiriki wa kanisa, familia na majirani.
Sikiliza na Uitike: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa na nyimbo.
Mapendekezo ya Nyimbo
- Namwandama Bwana (Vk. 336 & Vd. 128)
- Ni Wako Bwana (Vk. 159 & Vd. 144)
