Utupe Leo Riziki Yetu
Fungu Elekezi: “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio” (Gal. 6:9, 10).
Mungu Atatoa
Siku moja nilitumia muda kushughulikia mipango inayohusiana na fedha. Baada ya kutenga zaka yetu na asilimia ndogo kwa ajili ya utume na wahitaji, nililipa bili zote, nikatenga baadhi kwa ajili ya karo ya shule ya vijana wetu na kuwa na sehemu ndogo iliyobaki kwa muda uliobaki wa mwezi kwa ajili ya chakula na gharama nyinginezo. Niliingia kwenye gari letu ili nipeleke fedha za karo hadi shuleni na kuondoka. Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha.
Kabla tu ya kuingia kwenye barabara kuu ya shule, nilimwona mwanamama mmoja akionekana kuwa na huzuni. Nilisimamisha gari na kugundua kuwa ni mwanamama ambaye nilikuwa nimembatiza miezi michache tu iliyokuwa imepita. Alikuwa akilia.
“Kuna tatizo gani?” niliuliza. Hatimaye alieleza kwamba yeye, pamoja na wengine wengi, alikuwa amepoteza kazi wakati kiwanda cha jirani kilipofungwa. Kisha yeye, pamoja na watoto wake wawili wadogo, alifukuzwa katika nyumba yake kwa kuwa hakuweza kulipa kodi. Na sasa hawakuwa na chakula tena.
Nilimpeleka kwenye duka la vyakula na kujaza chakula kwenye mkokoteni, nikilipa kwa kutumia sehemu ya karo ya shule. Katika kumrudisha shuleni, nilimpigia simu mwenye nyumba na kwa shida nilifanikiwa kufanya makubaliano naye ambapo nilitumia fedha ya karo
iliyobaki kulipa nusu ya deni lake na mwenye nyumba alisamehe nusu nyingine. Niliwapigia simu wajumbe wa baraza la kanisa na walilipa bili ya umeme. “Pia,” nikasema, “baada ya kusimama, msaidie mtu mwingine aliye na uhitaji.” Alishukuru sana.
Nilipofika nyumbani na kumwambia mke wangu kwamba nilikuwa nawaza jinsi tutakavyolipa karo, alisema kwa shangwe, “Mungu atatoa.” Mchana ule nilipoangalia sanduku la barua, nilipata bahasha yenye hundi ndani yake. Ni kiasi kile kile nilichotumia kumsaidia yule mwanamama.
Mungu anatujali sana zaidi ya vile tunavyowajali watoto wetu. Anaahidi kwamba atatulisha (Isa. 33:16). Lakini zingatia neno utupe kwenye aya: “utupe leo riziki yetu.” Kwa uwazi kabisa Yesu anatudokeza kwamba tusiombe tu kwa ajili yetu bali pia kwa ajili ya wale wanaotuzunguka. Kwa kweli, Biblia iko wazi kabisa kwamba sharti tuwapende wengine kama vile tunavyojipenda (Marko 12:31), na lazima tuombe kwa ajili ya wengine (Yakobo 5:16). “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo” (Gal. 6:2). Wanafunzi wa karne ya kwanza walifanya hivyo. Walikuwa wamoja katika kila kitu walichokifanya (Matendo 4:32).
“Sala zetu hazipaswi kuwa ombi la ubinafsi, kwa faida yetu wenyewe. Tunapaswa kuomba ili tuweze kutoa. Kanuni ya maisha ya Kristo lazima iwe kanuni ya maisha yetu…. Tunapaswa kuomba baraka kutoka kwa Mungu ambazo tunaweza kuzifikisha kwa wengine. Uwezo wa kupokea hupokelewa tu kwa kutoa. Hatuwezi kuendelea kupokea hazina za mbinguni bila kuziwakilisha kwa wale wanaotuzunguka” (Christ’s Object Lessons, uk. 142, 143).
Zingatia kwamba sala ya Bwana haizungumzi kuhusu riziki kwa ajili ya kesho, ni kwa ajili ya leo tu. Wana wa Israeli waliweza kuokota mana kwa ajili ya siku moja tu (Kut. 16:4). Mungu hataki usumbukie ya kesho (Mt. 6:34). Omba kwa ajili ya leo. Omba ili uwasaidie wengine. Tafuta kuwabariki. Kabla wafuasi wa Yesu hawajahubiri, wanapaswa kuonesha upendo wao kwa Mungu kwa kuwa mbaraka kwa wale wanaowazunguka.
Katika hukumu Yesu hatauliza kama ulienda kanisani au ulifanya mambo mengine mazuri, ingawa hatupaswi kuacha kukusanyika(Ebr. 10:25). Atasema, “Nalikuwa ni uchi na mwenye njaa na kiu. Jinsi ulivyowapenda wale waliokuzunguka inaonesha jinsi ulivyonipenda” (tazama Mt. 25:31–45).
Mungu anakuita ili uombe kwa ajili ya jirani yako, mpende jirani yako na uwe mbaraka kwa wote wanaokuzunguka.
Hebu Tuombe Pamoja
Muda wa Maombi (Dakika 30–45)
Vikundi vyote vya maombi vina njia tofauti za kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja, kwa njia yo yote ambayo Roho Mtakatifu anaongoza. Tunahimiza maombi mafupi ya wazi (sentensi 1-3). Hii inaruhusu watu wengi zaidi kuomba mara nyingi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuomba kupitia Maandiko kulingana na mada. Unaweza kuomba kupitia vifungu vingine pia na kujumuisha masomo mengine katika wakati wako wa maombi. Tazama Mwongozo wa Kiongozi na Maombi ya Maombi ya Kanisa Ulimwenguni kwa mawazo ya maombi.
Kuomba Sawasawa na Neno la Mungu—Wagalatia 6:9, 10.
“Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.”
“Hebu Tusichoke katika Kutenda Mema”
Baba, wakati mwingine huduma hutuacha tukiwa tumechoka. Tunazingatia sana mipango na matokeo na kusahau kuwa Wewe ndiye Chanzo cha nguvu zote. Tafadhali elekeza macho yetu kwako. Ufufue roho zetu na utujaze na upendo Wako usioisha kwa ulimwengu wenye uhitaji.
“Tutavuna kwa Wakati Wake, Tusipozimia Roho”
Bwana, asante kwa ahadi hii kwamba siku ya mavuno inakuja. Ifanye mikono yetu kuwa ya uaminifu tunapopanda na kumwagilia mbegu za imani kwa wengine. Matokeo ni juu yako!
“Tuwatendee Watu Wote Mema”
Mungu wetu, tunaomba utupatie macho ili tuone fursa kwa ajili ya huduma. Tuoneshe jinsi ambavyo tunaweza kuonesha upendo kwa watoto wetu, wenzi wetu, jirani zetu na kwa washiriki wenzetu kanisani. Tunafurahi sana kuwa sehemu ya familia ya Mungu!
Mapendekezo ya Maombi Zaidi
Shukrani na Sifa: Shukuruni kwa baraka mahususi na Msifuni Mungu kwa wema Wake.
Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na umshukuru Mungu kwa msamaha Wake.
Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.
Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).
Mahitaji ya Eneo Mahalia: Ombea mahitaji ya sasa ya washiriki wa kanisa, familia na majirani.
Sikiliza na Uitike: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa na nyimbo.
Mapendekezo ya Nyimbo
- Kuwatafuta Wasioweza (Vk. 195 & Vd. 100)
- Twapanda Mapema (Vk. 193 & Vd. 55)
- Walio Kifoni (Vk. 202 & Vd. 56)