SIKU 10 ZA MAOMBI – 2025
Neno kuu; BALI WEWE USALIPO
Siku ya kwanza: KAENI NDANI YANGU

Fungu Elekezi: “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote” (Yohana 15:5).

Kudumu Kuunganishwa—Hitaji kwa Ajili ya Kuzaa Matunda
Baada ya kuhitimu niliitwa kutumika kwenye mtaa wenye makanisa madogo matatu. Ulikuwa ni wakati wa majira ya baridi. Moja ya makanisa lilikuwa na washiriki wazee. Katika kila Sabato hasa yenye tukio maalum, tulikuwa na watu takribani 40. Kwenye Sabato ya kawaida tulikuwa na watu takribani 10.

Sabato moja kulikuwa na baridi sana, ilikuwa takribani nyuzi joto -30 na watu tisa walihudhuria: familia yangu ya watu wanne na wengine watano. Niliwaza, je, nihubiri? Mzee kiongozi wa kanisa, mwanamke ambaye alikuwa na umri wa takribani miaka 90, alisema, “Tunarudisha zaka, kwa hiyo inakulazimu kuhubiri.” Kwa hiyo nilihubiri.

Hubiri langu lilitoka katika kitabu cha Yohana 15:4–8. Katika aya nne Yesu anarudia “Kaeni ndani Yangu” mara tatu. Katika utamaduni wa Kiebrania, jambo linaporudiwa mara tatu ni muhimu sana yaani muhimu mno. Nilisisitiza kwamba cha muhimu sana si kile tunachokifanya katika maisha ya Kikristo. Tunapoitwa kutumika, hatuwezi kuwa na matokeo kwa uwezo wetu wenyewe. Hata hivyo Yesu alitoa Neno Lake kwamba ikiwa tutadumu kukaa ndani Yake, chochote tutakachoomba, tutatendewa. Hakuna utata; ni uthibitisho wa mafanikio kwa asilimia 100.

“Kwa hiyo,” niliwaambia wasikilizaji, “si kile tunachofanya kiletacho mabadiliko, bali kile ambacho Mungu anaweza kufanya.”

Mwandishi Ellen G. White anaeleza, “Si uwezo ulio nao sasa, au utakaowahi kuwa nao, utakaokupa mafanikio. Ni yale ambayo Bwana anaweza kufanya kwa ajili yako. Tunahitaji kuwa na imani kidogo mno katika kile ambacho mwanadamu anaweza kufanya, bali kuwa na imani zaidi katika kile ambacho Mungu anaweza kufanya kwa kila nafsi inayoamini” (Christian Service, uk. 262).

Niliwaambia kusanyiko langu dogo kwamba maombi “ni siri ya kuwa na nguvu za kiroho” (Prayer, uk. 12). “Yanatuunganisha na (Chanzo cha nguvu” (Steps to Christ, uk. 95). “Ni silaha yenye ufanisi zaidi dhidi ya mashambulizi ya Shetani” (Testimonies for the Church, vol. 1 uk. 295, 296, 345, 346).

Niliwaambia juu ya ahadi ambayo Yesu aliitoa katika Mathayo 18:19, 20. “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.” Haisemi “ikiwa 200 au 300 wataomba” bali “ikiwa 2 au 3 wataomba” kwa ajili ya jambo fulani kwa mapatano, katika umoja. Na sio “Ninaweza nikalifanya” bali kwa uwazi kabisa “Nitalifanya.”

Niliwaambia wasikilizaji wangu wachache, “hatuwezi kuchagua kutofanya kitu. Lazima tuombe na kufanya kazi, kisha Mungu ataleta matokeo kama alivyoahidi.” Lilikuwa hubiri bora juu ya nguvu ya maombi.

Tulipokuwa tukirudi nyumbani, nilimwambia mke wangu, “Tunahitaji kuhama. Hakuna tumaini la ukuaji au kwa kweli wa kitu chochote katika kanisa hili.” Alinikumbusha hubiri langu, kwa ahadi ya Yesu, na kisha akaniuliza, kwa nini usiwaite katika maombi?” Nilisita kufanya hivyo. Wale wanawake wachache walikuja kila asubuhi saa 12:30 asubuhi. Ili kuomba pamoja kwa ajili ya Roho Mtakatifu, ukuaji wa kanisa, familia, jiji, mpango wa Mungu kwa kanisa letu na uwazi kwa kile tunachotaka kukifanya. Miezi mitatu baadaye kanisa lilikuwa na watu waliohudhuria takribani 120.

Mungu anakuita ili udumu ndani Yake, omba bila kukoma, baki ukiwa umeunganishwa na kutembea Naye. Anakualika ukae ndani Yake, na lazima kila siku umkaribishe akae ndani yako. Hicho ndicho chanzo chako pekee cha nguvu ya kweli. Huo ndiyo usalama wako. Maadamu umeunganishwa na Mungu, Shetani hana nguvu juu yako. Kristo ndani yako na wewe ndani Yake ni njia moja ya kukua na kufanikiwa.

Tuombe pamoja.
Muda wa Maombi (Dakika 30–45)
Vikundi vyote vya maombi vina njia tofauti za kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja, kwa njia yoyote ambayo Roho Mtakatifu anaongoza. Tunahimiza maombi mafupi ya wazi (sentensi 1-3). Hii inaruhusu watu wengi zaidi kuomba mara nyingi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuomba kupitia Maandiko kulingana na mada. Unaweza kuomba kupitia aya zingine pia na kujumuisha masomo mengine katika wakati wako wa maombi. Tazama Mwongozo wa Kiongozi na Maombi ya Maombi ya Kanisa Ulimwenguni kwa mawazo ya maombi.

Kuomba Sawasawa na Neno la Mungu—Yohana 15:5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”

“Kaeni Ndani Yangu Nami Ndani Yenu”
Bwana Yesu, tunaomba utufundishe namna ya kukaa ndani Yako kila siku. Pasipo Wewe, sisi ni kama matawi yaliyokufa kwa kutenganishwa kutoka kwenye mzabibu utoao uzima. Tembea pamoja nasi, fanya kazi ndani yetu, zungumza kupitia sisi. Tunaomba uishi ndani ya mioyo yetu na Uupende ulimwengu kupitia kwetu.

“Mtazaa Matunda Mengi”
Bwana, tunajua kwamba haki yote yatoka Kwako. Otesha tunda la Roho katika maisha yetu. Tujaze na upendo Wako, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu upole na kiasi. Ruhusu maisha yetu yaakisi tabia Yako isiyo na waa kwa kila mtu tunayekutana naye.

“Pasipo Mimi Hamwezi Kufanya Neno Lolote”
Bwana, tunajua kwamba matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi. Tunavunja ahadi zetu, tunawaudhi adui zetu, na kuwasaliti wale tunaowapenda. Pasipo Wewe, sisi tu wanyonge na waliopotea. Tunahitaji upendo Wako, uvumilivu Wako na neema Yako mioyoni mwetu kila siku. Tutunze karibu katika upande Wako.

Mapendekezo ya Maombi Zaidi
Shukrani na Sifa: Shukuruni kwa baraka mahususi na Msifuni Mungu kwa wema Wake.

Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na umshukuru Mungu kwa msamaha Wake.

Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.

Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu:

  1. Bwana, tunaomba uruhusu ule uamsho wa ucha Mungu wa zamani ulikumbe kanisa Lako katika siku hizi za mwisho. Tuwezeshe kusimama hata kama mbingu zianguke. Ruhusu uamsho huu uanze na mimi.
  2. Bwana tunaomba utuweze kuwa thabiti katika maombi kila siku, kwa mtu binafsi na kwa familia.
  3. Bwana, tunaomba utufungue macho yetu ili kuona uharibifu maishani mwetu. Mambo ambayo yanatuzuia tusiweze kukaza macho yetu Kwako. Tupatie mioyo ya kupenda kukuabudu Wewe tu.
  4. Bwana, tunaomba utusaidie tukuruhusu Wewe kutuamsha kila siku asubuhi, bila kujali ni mapema kiasi gani, ili kwamba tuweze kuwa na muda mzuri pasipo haraka katika Neno Lako na maombi.
  5. Tunaomba kwamba utuwezeshe kukujia jinsi tulivyo, kwa hisia zetu zote, mapungufu yetu, dhambi zetu, mahitaji yetu na tukuruhusu Utupende, utubadilishe na kutuumba upya ukitufanya kuwa vile Upendavyo tuwe.
  6. Bwana, tufundishe namna ya kuomba kila siku kwa ajili ya ubatizo wa Roho Mtakatifu.

Mahitaji ya Eneo Mahalia: Ombea mahitaji ya sasa ya washiriki wa kanisa, familia na majirani.

Sikiliza na Uitike: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa na nyimbo.
Mapendekezo ya Nyimbo za Kristo:

  1. Kaa Nami (19 Vk & 91 Vd)
  2. Ni Wako Bwana (159 Vk & 144 Vd)
  3. Moyoni (400 Vk & 211 Vd)
    🙏🙏🙏

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *