SIKU 10 ZA MAOMBI MWAKA 2025
Neno kuu; BALI WEWE USALIPO
Siku ya Pili: UTUFUNDISHE KUOMBA

Fungu elekezi: “Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, ‘tufundishe sisi kusali’” (Luka 11:1).

Moyo wa Uhai wa Mkristo

Maombi ni muhimu, tena ni uhai.
“Kila asubuhi tumia muda ili kuanza kazi yako kwa maombi. Usifi kiri kuwa muda huu ulipotea, ni muda utakaodumu hata milele. Kwa njia hii mafanikio na ushindi wa kiroho utapatikana” (Testimonies for the Church, vol. 7, uk. 194).

Mara nyingi wanafunzi walimshuhudia Yesu akiomba. Waligundua kuwa alikuwa na maisha ya maombi tofauti na ya kwao. Wanafunzi hawa walikuwa watu wema wa kiroho. Walikuwa wameisalimisha mioyo yao na walitaka kumtumikia Mungu. Walienda kanisani, waliitunza Sabato, walirudisha zaka kwa uaminifu na walikula chakula kisicho najisi. Kila mtu huko Israeli, hususani wanafunzi, alijua kuomba, sawa?

Tunadhani tunajua kuomba. Hata watoto wanajua kuomba. Lakini wanafunzi walipomtazama Yesu akiomba—na walipolinganisha maombi yao na ya Kwake—waligundua kuwa hawakujua jinsi ya kuomba. Hiyo ndiyo sababu iliyowafanya kusema, “Tufundishe kuomba” (Luka 11:1).

Tunafikiri kwamba kuomba ni jambo rahisi mno. Na ni kweli, Mungu atasikiliza ombi rahisi kabisa. Lakini lazima tuendelee kuimarisha maisha yetu ya maombi.

Wanafunzi waligundua kwamba walihubiri, lakini hakuna mtu aliyeguswa. Walijaribu kuponya au kutoa mapepo, lakini hawakuwa na nguvu. Walimwuliza Yesu, “Je! Wewe unafanyaje?” Yesu alisema, “Kwa kufunga na kuomba.”

Kimsingi Yesu anasema huwezi kufanya mambo kwa hekima yako mwenyewe; ni kwa nguvu ya Mungu tu. Ili uweze kufanikiwa, unapaswa kuomba kwa bidii. Katika kitabu cha Warumi, Paulo anasema kwamba lazima Roho Mtakatifu aombe kwa ajili yetu kwa sababu hatujui hata jinsi ya kuomba (Rum. 8:26).

Maombi ni pumzi ya nafsi. Ni siri ya nguvu za kiroho…. Puuza kufanya maombi, au jihusishe katika maombi kwa kushtukizwa, hapa na pale, kama ionekanavyo kuwa sawa, hapo utapoteza muunganiko wako na Mungu” (Prayer, uk. 12, 13).

Yesu alikuwa na maisha ya maombi yenye nguvu na mara nyingi alitumia usiku kucha katika maombi. “Yesu Mwenyewe, alipoishi miongoni mwa wanadamu, mara nyingi alikuwa katika maombi…. Yeye ni kielelezo chetu katika mambo yote…. Ubinadamu Wake uliyafanya maombi kuwa ni hitaji na fursa. Alipata furaha na faraja katika kujumuika na Baba Yake. Na ikiwa Mwokozi wa wanadamu, Mwana wa Mungu, alihisi hitaji la kuomba, ni jinsi gani basi wanadamu wanyonge, watendao dhambi wanapaswa kuhisi umuhimu wa maombi ya bidii na ya kudumu” (Steps to Christ, uk. 93, 94).

Yesu alifanya maombi kuwa kipaumbele Chake, kitu cha kwanza kabla siku haijaanza. “Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko” (Marko 1:35). Yesu alikuwa na muda na mahali kwa ajili ya maombi.

Wanafunzi waliposema, “Tufundishe kuomba,” Yesu hakuwaambia, “Ombeni kwa kusema hivi,” kama mantra (maneno ya kurudiarudia). Kwa kweli, aliwaambia waziwazi kwama wasirudierudie maneno yaleyale kila mara walipoomba (Mt. 6:7). Yesu Mwenyewe aliomba ombi tofauti katika Yohana 17, kulingana na hitaji la hali halisi.

“Maombi ni ufunguaji wa moyo kwa Mungu kama kwa rafi ki” (Steps to Christ, uk. 93). Katika maombi tunafungua mioyo yetu kwa Mungu katika mazungumzo ya kweli, kama majadiliano. Ikiwa unarudia maneno yayo hayo kila mara unapoomba, itakuwa desturi na wala hautakuwa unafi kiria kile unachokisema.

Maombi na usomaji wa Neno lazima viende pamoja daima. Kwa njia ya maombi tunaongea na Mungu; kwa njia ya Neno Mungu anaongea na sisi.

Yesu aliishi maisha ya maombi. Aliomba alfajiri na mapema, Alienda mahali maalum kwa ajili ya maombi, na alizungumza kwa uwazi na Mungu. Yeye ni kielelezo chetu. Anatuita ili tuombe kama Yeye.

Hebu na Tuombe Pamoja.

Muda wa Maombi (Dakika 30–45) Vikundi vyote vya maombi vina njia tofauti za kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja, kwa njia yoyote ambayo Roho Mtakatifu anaongoza. Tunahimiza maombi mafupi ya wazi (sentensi 1-3). Hii inaruhusu watu wengi zaidi kuomba mara nyingi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuomba kupitia Maandiko kulingana na mada. Unaweza kuomba kupitia aya zingine pia na kujumuisha masomo mengine katika wakati wako wa maombi.

Kuomba Sawasawa na Neno la Mungu—Luka 11:1 “Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, ‘tufundishe sisi kusali’”

“Yesu Alikuwa akiomba mahali fulani”
Baba, tunaomba utufundishe kuomba kama vile Yesu. Tunakiri kuwa na visingizio na kukengeushwa na kuwa na shughuli nyingi. Tusaidie kuchagua wakati na mahali pazuri pa kukutana Nawe kila siku. Badilisha vipaumbele vyetu na uunde tabia mpya zinazotuongoza katika uwepo Wako.

“Bwana, Tufundishe Kuomba” Ndiyo Bwana, tuoneshe namna ya kuomba kama ulivyowaonesha wanafunzi. Asante kwa mfano mzuri wa Sala ya Bwana. Tuoneshe jinsi ya kufanyiza maombi yetu na maisha yetu kwa mfano Wako. Tunaomba utujaze na Roho Mtakatifu, na usikie maombi yetu ili ubadilishe nyumba zetu, kanisa letu, jamii yetu na ufalme Wako.

Mapendekezo ya Maombi zaidi

Shukrani na Sifa: Shukuruni kwa baraka mahususi na Msifuni Mungu kwa wema Wake.

Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na umshukuru Mungu kwa msamaha Wake.

Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.

Kanisa Letu:

  1. Tunaomba kwa ajili ya mvua ya masika ya Roho Mtakatifu ili kuimarisha ushuhudiaji wetu na kutuwezesha ili kujihusisha katika kazi ambayo Umetupatia kabla ya ujio Wako.
  2. Tufundishe jinsi ya kuzipenda familia zetu kwa kujitoa kafara na namna ya kuwafanya wanafunzi kwa ajili ya Ufalme, kuanzia kwa watoto wetu na wapendwa wetu.
  3. Tunaomba utupatie hekima ya kulichunguza, kulielewa na kulitii Neno la Mungu. Tunaomba utufundishe kuyapambanua vyema maneno ya ukweli na kwa uaminifu kuwashirikisha wengine Neno Lako.
  4. Bwana, tunaomba uamshe upya hali yetu ya kuyathamini maagizo yanayopatikana katika maandiko yaliyovuviwa ya Ellen G. White.
  5. Tunaomba kwa ajili ya uhuru wa dini na haki ya dhamiri ulimwenguni kote. Bwana, tunaomba ufungue milango kwa ajili ya utangazwaji wa Neno Lako katika maeneo yaliyofungwa. Mahitaji ya Eneo Mahalia: Ombea mahitaji ya sasa ya washiriki wa kanisa, familia na majirani. Sikiliza na Uitike: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa na nyimbo. Mapendekezo ya Nyimbo

  1. Saa Heri ya Maombi (Vk. 278 & Vd. 135)
  2. Bwana Sikia (Vk. 402)
  3. Yesu Kwetu ni Rafiki (Vk. 182 & Vd. 130)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *