Jina Lako Litukuzwe

Fungu Elekezi: “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:16).

Sisi ni Barua ya Wazi

Wakati fulani washiriki wa kanisa, pamoja na mchungaji, walijaribu kualika majirani kwenye baadhi ya matukio. Baadhi yao walikataa. Mchungaji aliuliza familia kadhaa alizokuwa akifahamiana nao kwa nini hawakutaka kuja. Kwa maneno tofauti wote walisema, “Ikiwa Ndugu

                     ni mshiriki hapo, ni bora tusije. Si mtu mwema wala hana upendo. Hana heshima wala aibu. Ni mdanganyifu, huwatendea vibaya wanyama wake wa nyumbani na ni mwenye hasira na mkorofi siku zote.” Washiriki wengi wanamsikitikia tu.

Sala ya Bwana inaanza na maneno, “Baba yetu uliye mbinguni.” Mungu si Mungu tu wa ulimwengu bali pia Anao uhusiano wa karibu na wa kina pamoja nasi. Kisha inaendelea, “jina Lako litukuzwe.” Neno la Kiyunani si hagios—likimaanisha “takatifu, tukufu, enye kustahili heshima”—bali hagiazo—likimaanisha “kutakasa.” Tunawezaje kumtakasa au kumfanya Mungu kuwa Mtakatifu wakati Yeye ni Mtakatifu?

Paulo anasema sisi ni barua inayosomwa na watu wote (2 Kor. 3:2). Katika 1 Wakorintho 4:9 anaandika, “kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia.”

Watu hawamwoni Mungu, wanatuona sisi. Mwenendo wetu wa kila siku unaweza kuwa wa kumtukuza Mungu na kumheshimu au unaweza kudhalilisha jina Lake na kuliwakilisha vibaya kanisa na kuleta athari mbaya kwa kazi Yake (Mt. 5:13–16).

Ingia katika uwepo wa Mungu kwa nyimbo za sifa na kisha umtambue kuwa ni Baba yako mpendwa. Badala ya kujizingatia wewe na mahitaji yako, kwanza mzingatie Mungu, tunza sana jina Lake na heshima Yake. Mungu angependa tuombe kwa ajili ya vitu vile ambavyo vitaleta heshima kwa jina Lake. Hatupaswi kamwe kujitukuza wenyewe; tunalazimika kumwomba Mungu kwa ajili ya neema na Baraka za kiroho, ili kwamba tuweze kulitukuza jina Lake katika tabia zetu. Mungu anahimidiwa, jina Lake linatukuzwa, pale watoto Wake wanapotoa katika maisha yao mwonekano wa tabia ya Yesu” (Manuscript 34, 1903, par. 15).

Omba jambo kama hili: “Baba, niwezeshe kukuheshimu katika yote nifanyayo leo. Niwezeshe kukuwakilisha vyema na kulibeba jina Lako ili kwamba watu wanaponiona wapate kukuimbia Wewe sifa. Niruhusu nitende kwa namna ambayo itawafanya watu kuona tabia ya Yesu katika matendo na maneno yangu yote.”

Pia, katika maombi yako taka tu mambo ambayo yatamletea Mungu heshima na kumfurahisha. 1 Yohana 5:14 inasema kwamba, “tukiomba kitu sawasawa na mapenzi Yake, Atusikia.”

Lazima tuombe katika Jina la Yesu, lakini hiyo ina maana kubwa zaidi ya kusema tu “katika Jina la Yesu.” Katika nyakati za Biblia, jina liliwakilisha tabia. Kuomba katika jina la Yesu ni kuomba kwa kuongozwa na mapenzi Yake, kuomba mambo ambayo yatamwakilisha Yeye na tabia Yake. Yakobo 4:3 anasema, “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” “Kuomba katika jina ya Yesu kuna maana sana. Kuna maana kwamba tunapaswa kuikubali tabia Yake, kumdhihirisha Roho Wake na kutenda kazi Zake” (Tumaini, seh. ya 2, uk. 280).

Yesu aliahidi kujibu maombi yetu ikiwa tunaomba katika Jina Lake, chini ya mapenzi Yake, na kwa ajili ya kitu ambacho kitamletea Mungu utukufu na heshima (Yohana 14:13, 14; 1 Yohana 5:14).

Na pale Mungu anapojibu maombi, hakikisha unamtukuza na kumhimidi Yeye. Hatupaswi kamwe kujichukulia utukufu sisi wenyewe. Shetani anajaribu kuuchukua utukufu wa Mungu kwa ajili yake mwenyewe. Kwa unyenyekevu, kwa moyo wa shukrani mkiri na kumtukuza Mungu kupitia maneno, matendo na maombi.

Tunapolalamika tunatoa ujumbe mbaya kumhusu Mungu wetu. Kwa namna hiyo tunasema kwamba Mungu si mwema, hajali, wala si mwaminifu kwa ahadi Zake. Furahini siku zote (1 Thes. 5:16; Fil. 4:4). Omba, nena na utende kwa namna ambayo itamletea heshima Mungu. Unawezaje kuamsha imani unapokuwa na mashaka? Unawezaje kuwataka watu wengine wamtukuze Mungu wakati wewe ni mwenye manung’uniko?

Maombi yetu ya dhati yanapaswa kuwa, “Baba yangu mpendwa wa mbinguni, ninaomba uniwezeshe kusema na kutenda kwa namna ambayo itakuwakilisha Wewe kikamilifu kwa wengine. Ninaomba unipatie tu yale mambo ambayo yatakuletea Wewe utukufu na unisaidie kuyatumia kwa namna ambayo itakuletea heshima. Niruhusu nilitukuze jina Lako leo.”

Muda wa Maombi (Dakika 30–45)

Vikundi vyote vya maombi vina njia tofauti za kuomba pamoja. Tunawahimiza kutumia dakika 30-45 zinazofuata katika maombi ya pamoja, kwa njia yoyote ambayo Roho Mtakatifu anaongoza. Tunahimiza maombi mafupi ya wazi (sentensi 1-3). Hii inaruhusu watu wengi zaidi kuomba mara nyingi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya kuomba kupitia Maandiko kulingana na mada. Unaweza kuomba kupitia aya nyingine pia na kujumuisha masomo mengine katika wakati wako wa maombi. Tazama Mwongozo wa Kiongozi na Maombi ya Maombi ya Kanisa Ulimwenguni kwa mawazo ya maombi.

Kuomba Sawasawa na Neno la Mungu—Mathayo 5:16.

“Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”

“Nuru Yenu na Iangaze”

Bwana, Wewe ni chanzo cha nuru. Angaza kutokea ndani yetu ili wengine waweze kuona uzuri wa tabia Yako. Tuwezeshe kung’aa kwa mng’ao angavu na kwa ujasiri ili wengine wavutwe kwenye ufalme Wako kupitia upendo wetu.

“Wapate Kuyaona Matendo Yenu Mema”

Mungu wetu, mara nyingi tunasahau kwamba watu wengine wanatazama kila kitu tufanyacho. Wasaidie kuona upendo, siyo chuki maishani mwetu. Wasaidie kuona ukarimu si ubinafsi. Tenda maishani mwetu ili kuwabariki watoto wetu, jirani zetu na hata adui zetu.

“Wamtukuze BABA Yenu Aliye Mbinguni”

Mungu wetu, lazima wewe uongezeke na sisi tupungue. Tunyenyekeze na uwasaidie jirani zetu kuona nguvu na huruma Yako katika matendo yetu ya upendo.

Mapendekezo ya Maombi Zaidi

Shukrani na Sifa: Shukuruni kwa baraka mahususi na Msifuni Mungu kwa wema Wake.

Kuungama: Tumia dakika chache kwa ajili ya maungamo binafsi na umshukuru Mungu kwa msamaha Wake.

Uongozi: Mwombe Mungu akupatie hekima kwa changamoto na maamuzi ya sasa.

Kanisa Letu: Ombea mahitaji ya kanisa katika ngazi ya majimbo na kanisa la ulimwengu (tazama karatasi nyingine yenye mahitaji).

Mahitaji ya Eneo Mahalia: Ombea mahitaji ya sasa ya washiriki wa kanisa, familia na majirani.

Sikiliza na Uitike: Tumia muda kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitikia kwa sifa na nyimbo.

Mapendekezo ya Nyimbo

  • Bwana Mungu (Vk. 28 )
  • Nasifu Shani ya Mungu (Vk. 26 & Vd. 38)
  • Mwumbaji, Mfalme (Vk. 7 & Vd. 9)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *